Neno la Ukaribisho

Kwa niaba ya Menejimenti na Watumishi wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), ninayo furaha kuwakaribisha kwenye tovuti yetu iliyoboreshwa.Tovuti hii inawawezesha kupata taarifa za shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi yetu katika kukuza na kuendeleza Kiswahili Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Ni imani yangu  kuwa tovuti hii ni itakuwa njia sahihi inayowezesha jamii kupata taarifa muhimu zinazohusu BAKITA na shughuli zake. Miongoni mwa shughuli hizo ni; Usanifishaji, Mafunzo ya Kiswahili kwa Wageni, Mafunzo ya Msasa ya Ukalimani kwa Vitendo, Uhariri wa Miswada , Ithibati ya Vitabu na Miswada, Uandishi wa Vitabu na upatikanaji wake vikiwamo: Kamusi Kuu ya Kiswahili, Furahia Kiswahili, Mwongozo wa Taifa wa Ufundishaji Kiswahili kwa Wageni na vingine vingi. Aidha, Baraza linatoa huduma za Tafsiri, Ukalimani, Semina na Warsha kwa makundi mbalimbali kama vile Watumishi wa Umma, Waandishi wa Habari, Washereheshaji na Watu Binafsi.

Vilevile, kupitia tovuti hii, wadau, wapenzi na jamii kwa ujumla inapata elimu ya masuala mbalimbali yanayohusu matumizi fasaha na sanifu ya lugha ya Kiswahili.  Kiswahili ni lugha yetu ya Taifa na ni  lugha ya Afrika yenye mawanda mapana ya kutumika Kimataifa. Pia, Novemba 2021, nyota ya lugha hii ilizidi kung'ara baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuitengea siku maalumu ya kuadhimishwa duniani ambayo ni tarehe 7 Julai kila mwaka .

Ninatoa wito kwa wadau wote kuendelea kuitumia tovuti hii mara kwa mara na kuwasiliana nasi kwa maoni na ushauri kwa ajili ya kuboresha na kupata ufafanuzi zaidi kuhusu huduma zetu. “Hamadi kibindoni, silaha mkononi” na kwetu silaha ni Kiswahili.

Tujivunie na Kukienzi Kiswahili, Moja ya Tunu za Taifa Letu.

Consolata P. Mushi
KATIBU MTENDAJI