Maswali Yaulizwayo Mara kwa Mara

Kwa wale wanaotaka kutafsiriwa vyeti ni lazima watuletee nakala halisi na sio fotokopi. Kwa lugha ambazo Baraza lina wataalamu tunatafsiri kwa gharama ya Tsh 30,000 kwa cheti kimoja; Baraza linatumia wafasiri wa nje ambao wameidhinishwa kutafsiri lugha mbalimbali ambazo hatuna wataalamu wake ofisini.

Mtaalamu wa nje anatafsiri kwa gharama atakazoelewana na mteja na kuandika jina na saini yake kwenye tafsiri na kisha mteja atatakiwa kuleta BAKITA kwa ajili ya kuthibitishiwa kwa kugongewa muhuri. Gharama za kugonga muhuri ni Tsh 10,000 kwa Mtanzania na Dola za Marekani 20 au Tsh 40,000 kwa mteja asiye Mtanzania. Kwa tafsiri ya miswada, vitabu n.k tunatoza Tsh 30,000 kwa ukurasa mmoja wenye maneno kuanzia 200 hadi 220. Mteja atatakiwa kuleta nakala mango (hard copy) na nakala tete (soft copy) kama anayo. Baraza litampatia Ankara Kifani (Proforma Invoice) ambapo atatakiwa kulipa asilimia 50 ya malipo yote kabla ya kazi kuanza, na kisha anapokuja kuchukua kazi atatakiwa kukamilisha asilimia 50 iliyobakia kabla ya kukabidhiwa kazi.

Mtu, shirika, taasisi au Kampuni ambayo inapata shida katika kupata istilahi za Kiswahili zinazoendana na shughuli zake iwasilishe istilahi hizo BAKITA kwa njia ya simu, barua pepe na kwa njia ya barua za kawaida. Aidha, mtu binafsi anaweza kuja BAKITA kupata ushauri wa chochote kinachohusiana na maneno mbalimbali ya Kiswahili.

Ili kupatiwa ithibati ya muswada au kitabu chako, tafadhali fuata hatua hizi:

  1. Lete muswada wako katika nakala mango ofisini.

  2. Kurasa zitasemekana kwa malipo ya sh. 5,000 kwa kila ukurasa.

  3. Baada ya kulipia, utarudishiwa muswada ili kuingiza marekebisho yaliyopendekezwa.

  4. Rudisha tena muswada kwa uhakiki.

  5. Baada ya kuthibitishwa, muswada au kitabu kitagongwa muhuri rasmi na utapewa cheti cha uthibitisho kinachothibitisha kuwa lugha ni sahihi na inaweza kutumika kwa wadau husika.