Hatua ya Tatu
Kozi hii ni kwa ajili ya Kuboresha Ujuzi wa Kuzungumza Kiswahili, Kusoma, Kuandika na Kusikiliza katika Mazingira yasiyotabirika.
Kozi hii inatarajiwa kukuza uwezo wa mjifunzaji wa Kiswahili kuzungumza Kiswahili na kuendelea kupanua msamiati wa Kiswahili na maarifa ya sarufi. Atajizoeza kutumia sarufi changamani katika mazungumzo ya kila siku na kujumuisha misemo na nahau za kawaida za Kiswahili katika mazungumzo ya kila siku. Kwa muda wote, atahusika na makala, magazeti na matini za kiswahili zilizoteuliwa, kusikiliza habari na hotuba mbalimbali za kitaifa na kimataifa, kushiriki katika mijadala ya darasani, na kuandika insha, ripoti, na muhtasari wa habari. Kozi hii itamsaidia kujenga na kufahamu kanuni za sarufi ya Kiswahili, misemo na msamiati aliojifunza katika madarasa au masomo ya awali ya Kiswahili. Pamoja na shughuli za darasani, atashiriki katika ziara kadhaa za kimasomo na kiutamaduni na shughuli mbalimbali za kijamii zitakazomwezesha kuzamia kindakindaki katika mazingira ya lugha ya Kiswahili na utamaduni wake, na kuweza kukitumia Kiswahili katika mazingira yasiyotabirika.
MBINU
- Mkabala wa kimawasiliano
- Maigizo
- Ziara
- Kazi za vikundi
- Majadiliano
- Nyimbo
- Michezo ya lugha
- Vitu halisi
- Video/televisheni/sauti
- Uzamishaji
- Familia mwenyeji
- Rafiki wa lugha
- Mazoezi kwa vitendo
- Kumwalika mgeni
- Kazimradi
- Ujifunzaji wa Hiari
- Utafiti mdogo
- Mapitio ya machapisho mbalimbali
- Kazi za ubunifu
MJIFUNZAJI ATAJIFUNZA NINI?
Kuzungumza kuhusu mfumo wa huduma za uwekezaji nchini Tanzania na kulinganisha na nchi nyingine, Kuzungumza kuhusu mfumo viwanda na biashara nchini Tanzania kulinganisha na nchi nyingine, Kuzungumza kuhusu nishati na maendeleo nchini Tanzania, Kuzungumza kuhusu mabadiliko ya tabianchi nchini Tanzania, Kuzungumza kuhusu afya ya jamii, Kuzungumza kuhusu kuhusu madawa ya kulevya, Kuzungumza kuhusu utamaduni madhara ya utandawazi katika nchi zinazoendelea, Kuzungumza kuhusu michezo na utimamu wa mwili, Kuzungumza kuhusu Sanaa za maonesho za Tanzania ukilinganisha na mataifa mengine, Kikao cha kitamaduni, kinachozungumza juu ya tofauti kuu za tunu za jamii na maadili kati ya mataifa mbalimbali na Kuzungumza kuhusu utangamano wa jumuiya ya Afrika Mahsariki na uhusiano wa kimataifa.
WALENGWA WA KOZI HII NI WATU GANI?
Wale ambao wana tajriba muhimu ya kujifunza lugha ya Kiswahili na wana msamiati mpana na wamebobea katika dhana za kisarufi za kawaida.
