Kuhusu Sisi
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ni taasisi ya umma iliyo chini ya Wizara yenye dhamana ya Utamaduni. Baraza liliundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 27 ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya mwaka 1983 na 2016. Sheria hii inalipa Baraza mamlaka ya kusimamia maendeleo na matumizi ya Kiswahili na kuratibu shughuli za wadau wote wanaokuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baraza liliundwa kutokana na mapendekezo makuu ya Kamati iliyoundwa kwenye kikao cha wataalamu wa lugha kilichoitishwa na aliyekuwa Waziri wa Elimu Disemba, 1961. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuendeleza Kiswahili kama Lugha ya Taifa. Baraza lilianza kazi na watumishi wanne katika ofisi za Wizara ya Elimu. Mojawapo ya kazi za kwanza za Baraza ilipendekezwa iwe kutafsiri na kufasiri istilahi na misemo ya sheria.
Mwaka 1972, Baraza lilipata ofisi zake katika jengo la Shirika la Nyumba la Taifa, makutano ya mtaa wa Samora na Azikiwe jijini Dar es Salaam, na mwaka 2012 Baraza lilihamia katika ofisi mpya zilizopo Kitalu Na.45B, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
