TAPSEA YAHIMIZA WASHIRIKI WA MAFUNZO YA WWO KUWA MABALOZI WA MATUMIZI SAHIHI YA KISWAHILI

19 Nov, 2026
TAPSEA YAHIMIZA WASHIRIKI WA MAFUNZO YA WWO KUWA MABALOZI WA MATUMIZI SAHIHI YA KISWAHILI

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi Waendesha Ofisi Tanzania (TAPSEA), Bi. Halima Mbululo, amewahimiza washiriki wa mafunzo ya Matumizi ya Kiswahili Sanifu na Fasaha kwa Waandishi Waendesha Ofisi (WWO) kuwa mabalozi wa mafunzo hayo kwa viongozi na waandishi wenzao katika taasisi wanazofanyia kazi ili kuendeleza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli za kila siku za kiutendaji.

Bi. Mbululo ametoa wito huo alipokuwa akifungua mafunzo hayo yanayoandaliwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), yanayofanyika katika Hoteli ya Morena, mkoani Morogoro, kuanzia tarehe 16 hadi 21 Novemba 2026.

Katika hotuba yake, amewapongeza washiriki kwa kupata fursa ya kushiriki mafunzo hayo na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza maarifa watakayoyapata kwa kuyatumia katika maeneo yao ya kazi, pamoja na kuwahamasisha wengine kushiriki katika juhudi za kukuza Kiswahili ndani ya taasisi zao.

Aidha, ameeleza matarajio yake kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano baina ya BAKITA na TAPSEA katika kutekeleza dhamira ya kuhakikisha lugha ya Kiswahili inaendelea kuwa nyenzo muhimu ya mawasiliano na maendeleo katika shughuli za kazi.