Category Title
TANZANIA NA UNESCO KUSHIRIKIANA KUJENGA CHUO CHA KUHIFADHI NA KUENDELEZA LUGHA ZA KIAFRIKA
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), ipo katika mpango wa kujenga chuo maalumu jijini Dodoma kitakachojikita katika kuhifadhi, kulinda na kuendeleza lugha za Kiafrika.
Mhe. Makonda ameyasema haya baada ya kufanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa UNESCO anayeshughulikia Kipaumbele kwa Afrika na Uhusiano wa Nje, Lidia Arthur Brito, ambapo amesema mazungumzo yao yamezaa matokeo chanya na kugusia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na UNESCO katika sekta za Utamaduni, Elimu na Lugha.
Akizungumzia jitihada za kuifanya lugha ya Kiswahili itumike kwa upana zaidi katika majukwaa ya Kidijitali, Mhe. Makonda amesema amewasilisha kwa uongozi wa UNESCO suala la kuitaka kampuni ya Meta kuitambua rasmi lugha ya Kiswahili, ili shirika hilo liunge mkono juhudi za kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kupata nafasi kubwa zaidi katika mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali ya kimataifa.
