RAIS SAMIA AAGIZA KISWAHILI KUFUNDISHWA DUNIANI, VITUO VYA UTAMADUNI KUANZISHWA MATAIFA MBALIMBALI

07 Jul, 2026
RAIS SAMIA AAGIZA KISWAHILI KUFUNDISHWA DUNIANI, VITUO VYA UTAMADUNI KUANZISHWA MATAIFA MBALIMBALI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia suluhu hassan ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa ( BAKITA )na Baraza la Kiswahilj la Zanzibar ( BAKIZA )kushirikiana na Balozi za Tanzania duniani kuendeleza ufundishaji wa lugha ya Kiswahili na kuanzisha vituo vya Utamaduni wa Kiswahili katika Mataifa mbalimbali, ikiwamo Ufaransa.

Maelekezo hayo yaliwasilishwa leo, tarehe 07 Julai 2026, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, katika Makao Makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa, wakati wa kufunga Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani (MASKIDU) 2026.

Vituo hivyo vitakuwa majukwaa muhimu ya kuitambulisha na kueneza lugha ya Kiswahili, kuimarisha diplomasia ya utamaduni, pamoja na kufungua fursa za biashara na uwekezaji. Aidha, vitatoa nafasi kwa wananchi wa mataifa mbalimbali kujifunza historia, utamaduni, urithi na ustaarabu wa Kiafrika kupitia Kiswahili.

Amehimiza pia Watanzania wanaoishi ughaibuni (Diaspora )kuwarithisha watoto wao lugha ya Kiswahili ili kuendeleza utambulisho wa Taifa na kuhifadhi urithi wa kitamaduni kwa vizazi vijavyo.

Kadri Kiswahili kinavyoendelea kupata hadhi ya kimataifa, ndivyo utamaduni wetu utakavyoendelea kukua na lugha hiyo kuendelea kung’ara miongoni mwa lugha zenye ushawishi mkubwa duniani.