MAANDALIZI YA KONGAMANO LA PILI LA KISWAHILI LA KIMATAIFA YAPAMBA MOTO

01 Jun, 2026
MAANDALIZI YA KONGAMANO LA PILI LA KISWAHILI LA KIMATAIFA YAPAMBA MOTO

Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni (MUT) wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo, Bw. Bonifance Kadili, amewapongeza wanakikundi wa Magoma Moto Theatre Group cha Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa maandalizi mazuri wanayoyafanya kuelekea ushiriki wao katika Kongamano la Pili la Kiswahili la Kimataifa litakalofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 7 Julai 2026 katika Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), jijini Paris, Ufaransa.
Kikundi hicho kinatarajiwa kuwa miongoni mwa vikundi vya ngoma za asili vitakavyotoa burudani na elimu kwa washiriki wa kongamano hilo, likiwa sehemu ya jitihada za kuonesha uhusiano wa karibu uliopo kati ya lugha ya Kiswahili na utamaduni wake.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maandalizi ya kikundi hicho uliofanyika Tarehe 01/06/2026 katika ukumbi wa Taasisi hiyo, Bw. Kadili alisema kuwa ushiriki wa Magoma Moto Theatre Group katika kongamano hilo ni fursa muhimu ya kuitangaza Tanzania, utamaduni wake na lugha ya Kiswahili katika jukwaa la kimataifa.


"Kiswahili kinaendana na utamaduni wake. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha kuwa wageni na washiriki wa kongamano hili wanapata fursa ya kujifunza na kushuhudia urithi wetu wa kitamaduni kupitia sanaa za maonesho," asema Bw. Kadili.

Ukaguzi huo ni sehemu ya maandalizi yanayofanywa na Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Pili la Kiswahili la Kimataifa kwa lengo la kuhakikisha kuwa tukio hilo la kihistoria linafanyika kwa ufanisi, ubora na umakini mkubwa. Aidha, maandalizi hayo yanalenga kuendeleza, kuikuza na kuieneza lugha ya Kiswahili pamoja na kuutangaza utamaduni wa Mtanzania katika ngazi ya kimataifa.
Kongamano la Pili la Kiswahili la Kimataifa linatarajiwa kuwakutanisha wataalamu wa lugha, wanazuoni, wabunifu wa sera, wanafunzi, wanadiaspora na wadau mbalimbali wa Kiswahili kutoka sehemu tofauti duniani kwa lengo la kujadili maendeleo, fursa na mustakabali wa lugha ya Kiswahili katika karne ya 21.