Category Title
NTONDA ASISITIZA UBORA WA UFUNDISHAJI WA KISWAHILI KWA WAGENI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Methusela Ntonda, amesema kuongezeka kwa matumizi ya Kiswahili duniani kunatoa fursa kwa Tanzania kunufaika kiuchumi kupitia sekta za elimu, biashara na utalii, huku kukichochea ajira na uwekezaji katika ufundishaji wa lugha hiyo kwa wageni.
Akizungumza leo, Novemba 27, 2026, wakati wa kufunga warsha ya wamiliki wa vituo na walimu wa Kiswahili kwa wageni iliyofanyika katika Hoteli ya Morena, Morogoro, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha weledi wa walimu, matumizi ya teknolojia za kisasa na kuboresha mazingira ya kujifunzia ili kuongeza ubora wa mafunzo.
Aidha, amewataka wadau kuimarisha ushirikiano kati ya BAKITA, wamiliki wa vituo na walimu ili kuboresha ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni. Pia, amehimiza wamiliki wa vituo na walimu kuwasisitiza wajifunzaji kuwapeleka BAKITA kwa ajili ya kupima na kuthibitisha umahiri wao wa lugha kupitia Mtihani wa Kupima Umahiri wa Lugha ya Kiswahili unaotolewa na BAKITA.
