WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAUNGA MKONO MATUMIZI SANIFU YA KISWAHILI KUPITIA KAMUSI KUU YA KISWAHILI

06 May, 2026
WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAUNGA MKONO MATUMIZI SANIFU YA KISWAHILI KUPITIA KAMUSI KUU YA KISWAHILI

Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Mbaraka Stambuli, apokea Kamusi Kuu ya Kiswahili kutoka kwa Mchunguzi Lugha Mkuu wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Dkt. Rizati Mmary, leo Mei 6, 2026 katika Ofisi za Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Katika hatua ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha matumizi sanifu na fasaha ya lugha ya Kiswahili, Wizara hiyo imenunua jumla ya Kamusi Kuu za Kiswahili 20 kwa awamu ya kwanza kwa matumizi ndani ya taasisi hiyo.

Hatua hiyo inalenga kuongeza ufanisi wa matumizi ya Kiswahili katika shughuli za kiserikali hususan katika mawasiliano ya kikazi, uandishi wa nyaraka rasmi pamoja na utoaji wa huduma kwa umma. Aidha, ununuzi wa kamusi hizo unaonesha dhamira ya Wizara ya Katiba na Sheria katika kuendelea kukuza, kuhifadhi na kuenzi lugha ya Kiswahili kama sehemu muhimu ya utamaduni na utambulisho wa Taifa.

BAKITA linaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali katika kuhakikisha matumizi sahihi ya Kiswahili yanaimarishwa ili kukuza mawasiliano yenye uelewa mpana na yenye kuzingatia misingi ya Lugha Sanifu.