Kiswahili Chaendelea Kuvuka Mipaka: Maandalizi ya Kongamano la Pili la Kiswahili la Kimataifa Ufaransa Yashika Kasi

24 Jun, 2026
Kiswahili Chaendelea Kuvuka Mipaka: Maandalizi ya Kongamano la Pili la Kiswahili la  Kimataifa Ufaransa Yashika Kasi

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Anne Sophie Avé,  amekutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa, kwa niaba ya Waziri Mhe. Paul Christian Makonda leo Tarehe 24/06/2026, kujadili maandalizi ya Kongamano la Pili la Kiswahili la Kimataifa litakalofanyika nchini Ufaransa pamoja na kuimarisha Uhusiano na  ushirikiano kati ya Tanzania na Ufaransa.

 

Mazungumzo hayo yalijikita katika kuendeleza ushirikiano katika sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ikiwa ni pamoja na filamu na urithi wa kihistoria. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Katibu mkuu wa Wizara Bw. Methusela Ntonda, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni  Bw. Boniface Kadili, Bw Athumani Kiswagala kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) pamoja na viongozi kutoka taasisi mbalimbali zikiwamo Bodi ya Filamu Tanzania, BASATA, Bodi ya Michezo Tanzania,Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), TaSUBa na nyinginezo.