Category Title
KISWAHILI NA TEKNOLOJIA: HATUA MPYA YA KUIMARISHA MAWASILIANO
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limehitimisha mafunzo ya awamu ya pili ya Kiswahili Fasaha na Sanifu kwa Maofisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) leo tarehe 12 Juni 2026 katika ukumbi wa hotel ya Morena iliyopo Mkoani Morogoro. Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 8 hadi 12 Juni 2026 yalilenga kuimarisha uwezo wa Maofisa TEHAMA katika matumizi sahihi ya Kiswahili Sanifu na Fasaha katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mafunzo hayo yalijikita katika kuwajengea washiriki uelewa wa kanuni za matumizi ya lugha ya Kiswahili, uandishi wa kitaalamu, matumizi sahihi ya sarufi, pamoja na matumizi ya istilahi za TEHAMA zilizosanifiwa kwa Kiswahili. Lengo kuu lilikuwa kuhakikisha kuwa wataalamu hao wanatumia lugha ya Kiswahili kwa usahihi katika mawasiliano ya kikazi na utoaji wa huduma mbalimbali za kidijiti.
Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za BAKITA za kuendelea kukuza na kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili katika sekta mbalimbali za maendeleo, hususan katika kipindi hiki ambacho matumizi ya teknolojia yanaongezeka kwa kasi.
Aidha, yanaunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha Kiswahili kinatumika kikamilifu katika utoaji wa huduma na mawasiliano rasmi nchini.
Kupitia mafunzo hayo, BAKITA linaendelea kutekeleza wajibu wake wa kusimamia maendeleo ya lugha ya Kiswahili kwa kuhakikisha watumishi na wataalamu katika sekta mbalimbali wanapata maarifa yatakayowawezesha kutumia lugha hiyo kwa ufasaha, usahihi na ufanisi zaidi.
