Category Title
BALOZI WA KENYA NCHINI JAPAN ATEMBELEA BAKITA, ATOA MSUKUMO WA KIMATAIFA KWA KISWAHILI
Balozi wa Kenya nchini Japan Mheshimiwa Arthur Andambi, ambaye pia ni mdau wa Kiswahili na shughuli za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), alitembelea BAKITA katika ofisi zake zilizopo Kijitonyama, Makumbusho jijini Dar es Salaam tarehe 17 Aprili 2026.
Ziara hiyo ilianza saa nne asubuhi katika ukumbi wa mikutano wa BAKITA, ambapo Mheshimiwa Andambi alipata fursa ya kukutana na watumishi wa baraza hilo na kufanya mazungumzo mafupi yenye lengo la kubadilishana mawazo kuhusu maendeleo na uenezi wa lugha ya Kiswahili.
Katika ziara hiyo, balozi Andambi alisisitiza umuhimu wa kukuza Kiswahili katika ngazi ya kimataifa hususan katika nyanja za diplomasia, elimu na mawasiliano ya kimataifa. Aidha, alieleza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwamo BAKITA katika kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili duniani.
Hata hivyo, Kama sehemu ya shukrani pamoja na utekelezaji wa mpango wa Baraza wa kueneza na kukuza lugha ya Kiswahili, Mheshimiwa Andambi alizawadiwa vitabu mbalimbali vya Kiswahili ambavyo ni: Furahia Kiswahili, Mwongozo wa Taifa wa Ufundishaji wa Kiswahili kwa Wageni (Hatua ya Awali, Kati na Mwisho), Kamusi ya Kiswahili kwa Shule za Msingi pamoja na Kamusi Kuu ya Kiswahili.
Ziara hiyo imekuwa ya manufaa makubwa kwa Baraza, ikiakisi mshikamano na juhudi za pamoja katika kukuza na kueneza Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya Nchi.
