Category Title
SERIKALI YATOA WITO KWA WATANZANIA KUJENGA UTAMADUNI WA KUSOMA VITABU
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kujisomea vitabu ili kuongeza maarifa na kukuza uwezo wa kufikiri. Ametoa wito huo leo, Oktoba 12, 2026, alipokuwa akifungua rasmi maonesho ya 33 ya Kimataifa ya vitabu Tanzania yanayofanyika katika uwanja wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo yameandaliwa na Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA) kwa lengo la kutoa fursa kwa wadau wa sekta ya vitabu kukutana, kutangaza na kuonesha machapisho yao, pamoja na kuhamasisha utamaduni wa kusoma miongoni mwa Watanzania. Maonesho hayo pia ni jukwaa muhimu la kuimarisha sekta ya uchapishaji na kusogeza vitabu karibu na wasomaji, hivyo kuchangia upatikanaji wa maarifa na maendeleo ya elimu nchini.
Mhe. Mwinjuma amesisitiza pia umuhimu wa kuwaenzi watunzi wa vitabu vya Kiswahili kwa kuwapatia tuzo zinazotambua mchango wao katika kukuza fasihi andishi pamoja na kuimarisha uchapishaji upya wa machapisho ili kazi zao ziendelee kupatikana kwa wasomaji.
Aidha, amezipongeza taasisi zilizo chini ya Wizara yake, ikiwamo Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), kwa juhudi zinazofanywa katika kukuza lugha na fasihi ya Kiswahili, huku akihimiza Watanzania kufanya usomaji wa vitabu kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
