Category Title
SERIKALI YAIMARISHA MATUMIZI YA KISWAHILI SANIFU NA FASAHA KWA UTOAJI WA HUDUMA BORA KWA WANANCHI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuimarisha matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha nchini kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), kwa kutekeleza jukumu lake la kukuza, kuendeleza, kusimamia na kuhimiza matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili. Katika kutekeleza azma hiyo, BAKITA imeendesha mafunzo kwa Waandishi Waendesha Ofisi (WWO), yaliyofanyika kuanzia tarehe 19 hadi 24 Oktoba 2026 katika Hoteli ya Isamilo Grand, mkoani Mwanza.
Mafunzo hayo yalilenga kuwaongezea washiriki ujuzi na stadi za kutumia Kiswahili sanifu na fasaha katika shughuli za kiofisi, hususan uandishi na uandaaji wa nyaraka rasmi, ili kuboresha mawasiliano na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Vilevile, mafunzo hayo yanatoa fursa kwa Waandishi Waendesha Ofisi kuwa mabalozi wa matumizi sahihi ya Kiswahili katika maeneo yao ya kazi kwa kuzingatia misingi ya usanifu na ufasaha wa lugha wanapotekeleza majukumu yao. Jitihada hizi zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha matumizi ya Kiswahili kwa weledi na ufanisi katika nyanja mbalimbali za kitaifa.
Kupitia mafunzo hayo, BAKITA inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kutekeleza jukumu lake la kukuza, kubidhaisha, kuendeleza, kusimamia na kuhimiza matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha nchini, ili lugha hiyo iendelee kuwa chombo madhubuti cha mawasiliano, utawala na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
