Category Title
BAKITA YAWAPOKEA WANAFUNZI NA WAHADHIRI KUTOKA USIU-AFRICA, KENYA
Dar es Salaam — Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limewapokea wanafunzi na wahadhiri kutoka United States International University–Africa (USIU), Kenya, tarehe 30 Julai 2026, waliozuru taasisi hiyo kwa lengo la kujifunza kuhusu lugha ya Kiswahili, historia yake na mchango wake katika kuunganisha Waafrika.
Katika ziara hiyo, wageni hao wameeleza kuvutiwa na ukarimu wa Watanzania, matumizi ya Kiswahili sanifu, pamoja na juhudi zinazofanywa na BAKITA katika kukuza lugha hiyo ndani na nje ya nchi. Wamebainisha kuwa Kiswahili ni miongoni mwa lugha za Kibantu, ni urithi wa Waafrika wote na ni nyenzo muhimu ya kuimarisha umoja wa bara la Afrika.
Akizungumza kuhusu uzoefu wake, mwanafunzi wa USIU, Joan Kemunto Nyamweya, amesema amefurahishwa na ukarimu na upole wa Watanzania, akieleza kuwa Kiswahili kinachozungumzwa Tanzania ni sanifu zaidi kikilinganishwa na Kenya, ambako lugha hiyo huchanganywa mara kwa mara na Kiingereza au Kisheng.
“Nimefurahia sana ukarimu wa Watanzania, vyakula vyao kama mishikaki ya nyama, nimejifunza mengi kwa Watanzania — kikubwa ni ukarimu na upole wao. Kwa upande wa lugha, Watanzania ni wenye lugha sanifu ya Kiswahili tofauti na Kenya ambako tunachanganya sana Kiswahili na Kiingereza au Kisheng.” Joan Kemunto Nyamweya, Mwanafunzi — USIU
Naye, Simon Egete Maraka (mwanafunzi), amesema amefurahi kujua kuwa BAKITA inakuza Kiswahili si Tanzania pekee bali popote ambapo ubalozi wa Tanzania upo duniani, akitamani hatua kama hiyo ichukuliwe pia nchini Kenya.
“Nimefurahi kufika Tanzania. Nimejifunza kuwa BAKITA ni taasisi inayokuza Kiswahili si hapa tu Tanzania bali kila mahali ambapo ubalozi wa Tanzania upo. Ninapenda hatua hii, huenda hata Kenya tungekuwa nayo ili kuendeleza jitihada kama za BAKITA.” Simon Egete Maraka, Mwanafunzi — USIU
Kwa upande wake, Abiba Achola Andeyi amesisitiza kuwa Kiswahili si lugha ya taifa moja bali ni mali ya jamii, ikitumika na kufundishwa katika vyuo vikuu vya mataifa mengi ya Afrika.
“Nimejifunza kwamba Kiswahili si lugha ya mtu mmoja, ni mali ya jamii — lugha ambayo mataifa mengi ya Afrika yanaitumia, vilevile mataifa mengi yanafundisha lugha hii katika vyuo vikuu.” Abiba Achola Andeyi, Mwanafunzi — USIU.
Mwanafunzi Joseph Owino ameeleza kuwa ziara yao Tanzania ilikuwa na lengo la kufanya utafiti kuhusu maisha ya Watanzania, na amefurahishwa na ukarimu, urafiki na uchangamfu wa wananchi. Ameongeza kuwa BAKITA imemfundisha asili ya Kiswahili na jinsi lugha hiyo ilivyopitia mchakato mrefu kufikia hapa ilipo sasa, akisisitiza umuhimu wa kuitumia kama lugha ya kimataifa itakayoimarisha umoja wa Waafrika.
“Tumekuja Tanzania kufanya utafiti kuhusu maisha ya Watanzania, na nimefarijika kwamba Tanzania ni nchi yenye watu wakarimu sana, marafiki na wacheshi sana. BAKITA wamenifundisha asili ya Kiswahili, na nimejifunza kuwa ni lugha ambayo imepitia mchakato wa muda mrefu ili kuwa hivi na hapa ilipo. Tunapaswa kuitumia kama lugha moja ya kimataifa ili itusaidie katika kuimarisha umoja wetu.” Joseph Owino, Mwanafunzi — USIU
Mhadhiri wa USIU, Prof. Hussein Abdullahi Mahomoud, ameeleza kuwa BAKITA ni “darasa tosha” kwa mataifa ya Afrika katika kujifunza namna ya kuendeleza Kiswahili, akisisitiza umuhimu wa lugha hiyo kuwa kiungo cha Waafrika wote.
“Watanzania ni wakarimu sana, ni nchi ambayo watu wake ni wakarimu kila pahala tunapoenda, hata kama hatuna miadi wametupokea na kutusikiliza. Tunatamani Kiswahili kuwa lugha ya bara la Afrika ili ituunganishe Waafrika. BAKITA ni darasa tosha kwa mataifa ya Afrika kujifunza namna gani zinapaswa kukifanya Kiswahili kuwa lugha moja inayounganisha Waafrika wote.” Prof. Hussein Abdullahi Mahomoud, Mhadhiri — USIU
Akizungumzia ziara hiyo, Mchunguzi Lugha Mkuu wa BAKITA, Edward Nnko, amesema BAKITA ni mdau mkubwa katika kueneza matumizi fasaha na sanifu ya Kiswahili, na kwamba kupokea wanafunzi hao kutoka Kenya ni fursa ya kuonesha kuwa Kiswahili ni lugha ya Kiafrika inayohitajika kwa Waafrika wote. Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Miaka 10 wa Kubidhaisha Kiswahili (2022–2032).
“BAKITA ni mdau mkubwa katika kueneza matumizi fasaha na sanifu ya lugha ya Kiswahili. Tumepokea wanafunzi kutoka nchini Kenya katika chuo cha USIU — hii kwetu ni fursa ya kuonesha kuwa Kiswahili ni lugha ya Kiafrika ambayo inahitajika kwa Waafrika wote, na ni hatua muhimu kwetu katika kutekeleza Mkakati wa Miaka 10 wa Kubidhaisha Kiswahili 2022/2032.” Edward Nnko, Mchunguzi Lugha Mkuu — BAKITA
BAKITA imeeleza kuwa ziara hii ni ishara ya kukua kwa hadhi ya Kiswahili kimataifa, huku ikisisitiza kuwa Kiswahili si mali ya taifa moja bali ni sauti ya Afrika inayozidi kuvuka mipaka na kuunganisha watu wake.
