BAKITA YAPATA ELIMU KUHUSU MATUMIZI YA NISHATI SAFI NA SALAMA

30 Sep, 2026
BAKITA YAPATA ELIMU KUHUSU MATUMIZI YA NISHATI SAFI NA SALAMA

Watumishi wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) wamepata elimu kuhusu umuhimu na faida za matumizi ya nishati safi na salama, hususani matumizi ya umeme, ikiwa ni pamoja na mchango wake katika kupunguza moshi na uchafuzi wa mazingira. Tukio hilo limeongozwa na Mkurugenzi wa Maendeleo na Matumizi ya Lugha, Bw. Kulwa Abel Kindija, kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza, Bi. Consolata P. Mushi.

Akizungumza na watumishi wa BAKITA, Bw. Juma Msuya, Afisa Huduma kwa Wateja kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkoa wa Kinondoni, ameeleza kuwa matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia ni nafuu ikilinganishwa na baadhi ya aina nyingine za nishati, huku yakichangia kuboresha mazingira ya kupikia na kupunguza uchafuzi wa mazingira.

Aidha, Bw. Msuya amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama kutokana na faida zake katika kulinda mazingira, kuboresha afya na kuchangia ustawi wa jamii.

Elimu hiyo imetolewa leo tarehe 30 Septemba 2026, katika ukumbi wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Makumbusho, Dar es Salaam.

”Nishati safi ya kupikia okoa maisha na mazingira”