Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limekabidhi vyeti rasmi vya utambuzi kwa vituo viwili vya kufundisha Kiswahili kwa wageni, ambavyo ni Loashi Institute kilichopo Lumumba na Kiswahili Simplified kilichopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam. Hatua hii ni sehemu ya jitihada za BAKITA za kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili kwa kuzingatia ubora na viwango vya ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni.
Vyeti hivyo vilikabidhiwa na Maofisa wa BAKITA, Bw. Edward N. Nnko, Mchunguzi Lugha Mkuu na Mratibu wa Kitengo cha Kiswahili kwa Wageni pamoja na Bw. Omary J. Mchibya, Mchunguzi Lugha na Mkufunzi wa Kiswahili kwa Wageni.
Aidha, hatua hiyo ni mwendelezo wa dhamira ya BAKITA ya kuratibu, kusimamia na kuendeleza mazingira rasmi, salama na yenye viwango vya ubora katika ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni, sambamba na kuongeza idadi ya vituo vinavyotambuliwa rasmi kwa ajili ya kufundisha lugha hiyo nchini.