Category Title
BAKITA Yaweka Mkazo katika Kiswahili na Lugha ya Alama kwa Huduma Jumuishi kwa Wananchi
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limeendesha mafunzo ya Waandishi Waendesha Ofisi (WWO) yaliyoanza tarehe 21 Septemba 2026 katika ukumbi wa hoteli ya New Kiboko iliyopo jijini Tanga , mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea washiriki ujuzi wa matumizi fasaha na sanifu ya lugha ya Kiswahili kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Katibu Mtendaji wa BAKITA, Bi. Consolata P. Mushi, amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuwajengea Waandishi Waendesha Ofisi uwezo wa kutumia Kiswahili kwa usahihi na kuimarisha ujuzi wa Lugha ya Alama ili waweze kuwasiliana na kutoa huduma kwa ufanisi zaidi kwa wananchi wenye changamoto za kusikia na kuzungumza Hatua hii inalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma kwa usawa na bila vikwazo vya mawasiliano. Vilevile maarifa ya matumizi akiliunde katika Kiswahili yatawasaidia kuharakisha na kurahisisha majukumu yao ya kazi za kila siku hususan uhariri na uandishi wa vyaraka mbalimbali ili kuongoza ufanisi na tija katika taasisi.
Mafunzo hayo yanayofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 25 Septemba 2026 yanalenga kukuza huduma jumuishi katika taasisi, kwa kuwawezesha Waandishi Waendesha Ofisi kuwa na uelewa na stadi za msingi za Lugha kwa kuzingatia maadili katika mazingira ya kazi. Hatua hii inalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma kwa usawa na bila vikwazo vya mawasiliano na kuepusha migogoro.
Aidha, Bi. Mushi amewahimiza Waandishi Waendesha Ofisi ambao bado hawajapata mafunzo hayo kujisajili na kutumia fursa ya mafunzo yatakayoendelea kutolewa katika kanda mbalimbali nchini, ili kuongeza ujuzi, kuimarisha weledi na kuchangia katika kuboresha mawasiliano na utoaji wa huduma katika taasisi zao.
