Category Title
BAKITA YAENDELEA KUIMARISHA MATUMIZI YA KISWAHILI SANIFU NA FASAHA KATIKA SHUGHULI ZA KIOFISI
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limeendelea kutekeleza jukumu lake la kukuza, kuendeleza na kuhimiza matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha nchini kwa kutoa mafunzo kwa Waandishi Waendesha Ofisi (WWO), yaliyofanyika kuanzia tarehe 04 hadi 10 Oktoba 2026 katika Hoteli ya Isamilo Grand iliyopo mkoani Mwanza.
Mafunzo hayo yamelenga kuwaongezea washiriki ujuzi na stadi za kutumia Kiswahili sanifu na fasaha katika shughuli za kiofisi, hususan uandishi na uandaaji wa nyaraka rasmi, ili kuboresha mawasiliano na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia BAKITA za kuimarisha matumizi sahihi ya Kiswahili katika taasisi za umma na kuhakikisha lugha hiyo inaendelea kuwa nyenzo muhimu ya mawasiliano, utoaji wa huduma kwa wananchi na utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Vilevile, mafunzo hayo yanatoa fursa kwa Waandishi Waendesha Ofisi kuwa mabalozi wa matumizi sahihi ya Kiswahili katika maeneo yao ya kazi kwa kuzingatia misingi ya usanifu na ufasaha wa lugha wanapotekeleza majukumu yao. Jitihada hizi zinaonesha dhamira ya BAKITA ya kuhakikisha kuwa Kiswahili kinaendelea kutumika kwa ufasaha, weledi na ufanisi katika nyanja mbalimbali za kitaifa.
Kupitia mafunzo hayo, BAKITA inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kutekeleza jukumu lake la kukuza, kuendeleza, kusimamia na kuhimiza matumizi ya Kiswahili sanifu na fasaha nchini, ili lugha hiyo iendelee kuwa chombo madhubuti cha mawasiliano, utawala na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
