BAKITA YAENDESHA MAFUNZO YA KUIMARISHA STADI ZA KUFUNDISHIA KISWAHILI KWA WAGENI

21 Jul, 2026
BAKITA YAENDESHA MAFUNZO YA KUIMARISHA STADI ZA KUFUNDISHIA KISWAHILI KWA WAGENI

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) linaendelea kutekeleza jukumu lake la kukuza, kuendeleza na kueneza matumizi ya Kiswahili sanifu kupitia mafunzo ya Kuimarisha Stadi za Kufundishia Kiswahili kwa Wageni yanayowalenga walimu wa lugha hiyo.

 

Mafunzo hayo, yanayofanyika katika Ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Kijitonyama, Dar es Salaam, yalianza tarehe 20 Julai 2026 na yanatarajiwa kukamilika tarehe 31 Julai 2026.

 

Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki mbinu za kisasa za ufundishaji, kuimarisha umahiri wao katika uwasilishaji wa maudhui na kuongeza ubora wa ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni, sambamba na kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya kujifunza lugha ya Kiswahili duniani.

 

Mafunzo ya Kiswahili kwa wageni ni miongoni mwa huduma na majukumu ya msingi ya BAKITA katika kuendeleza na kuhimiza matumizi ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.

 

Mafunzo hayo yanaratibiwa na Bw. Edward N. Nnko, Mchunguzi Lugha Mkuu na Mratibu wa Mafunzo ya Kiswahili kwa Wageni BAKITA, kwa kushirikiana na Bw. Omary J. Machibya, Mchunguzi Lugha na Mkufunzi wa Kiswahili kwa Wageni ambao wanaendelea kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha ubora wa ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni nchini.

 

Kupitia mafunzo haya, BAKITA linaendelea kuimarisha hadhi ya Kiswahili kama lugha ya kimataifa kwa kuhakikisha walimu na wakufunzi wanapata stadi zinazowawezesha kufundisha kwa ufanisi, weledi na kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika kimataifa.