BAKITA NA BODI YA UTALII (TTB) TANZANIA KUSHIRIKIANA KATIKA KUKUZA KISWAHILI NA UTALII WA KIUTAMADUNI

27 Dec, 2025
BAKITA NA BODI YA UTALII (TTB) TANZANIA KUSHIRIKIANA KATIKA KUKUZA KISWAHILI NA UTALII WA KIUTAMADUNI

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),wamefanya kikao leo tarehe 16 Novemba,2025 kilichokuwa na lengo la kuanzisha ushirikiano wa kutoa mafunzo maalumu kwa wadau mbalimbali wa utalii kufunza Kiswahili kwa wageni wakiwemo watalii katika juhudi za kueneza Kiswahili na kukuza utalii wa kiutamaduni. 
Kikao hicho kililenga kuboresha uhusiano wa taasisi, kuunda mazingira chanya katika tasnia ya utalii pamoja na kuendeleza matumizi ya Kiswahili kwa wageni kama nyenzo muhimu ya mawasiliano, utamaduni na utambulisho wa Taifa.

Kikao hicho kimeongozwa na Bw. Francis Sangunaa, Mkurugenzi wa Huduma wa Bodi ya Utalii Tanzania, ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho na Katibu Mtendaji wa BAKITA, Bi. Consolata Mushi, aliwakilishwa na Bw. Athumani Kiswagala, ambaye alitoa shukrani zake kwa Bodi ya Utalii kwa kukubali mapendekezo ya BAKITA ya kushirikiana nao katika kukieneza Kiswahili na kukipa thamani yake kama moja ya tunu muhimu za Taifa.

Baada ya hayo, Bw. Edward Nnko, Mchunguzi Mkuu wa Lugha na Mratibu wa kitengo cha Kiswahili kwa Wageni BAKITA, aliwasilisha hoja ya BAKITA kuhusu mafunzo hayo, ambapo alieleza masuala mbalimbali ambayo yalijadiliwa kwa lengo la kuimarisha matumizi ya Kiswahili katika sekta ya utalii.

Kwa pamoja, BAKITA na TTB walionesha dhamira ya kuendeleza ushirikiano huo kwa vitendo, wakiamini kuwa Kiswahili ni rasilimali muhimu inayoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza utalii, ajira na uchumi wa taifa kwa ujumla.