BAKITA NA ALAF WASHIRIKIANA KUIMARISHA MATUMIZI YA KISWAHILI FASAHA NA SANIFU

21 Jul, 2026
BAKITA NA ALAF WASHIRIKIANA KUIMARISHA MATUMIZI YA KISWAHILI FASAHA NA SANIFU

Baraza la Kiswahili la Taifa BAKITA kwa kushirikiana na Aluminium African Limited (ALAF), wametoa Mafunzo Matumizi ya Kiswahili Fasaha na Sanifu kwa Waandishi wa Vitabu, Wahariri na Wachapishaji.

Mafunzo hayo yaliyofanyika leo tarehe 21 Julai 2026 katika Ukumbi wa BAKITA - Dar es salaam, yalifunguliwa na Mkurugenzi wa Maendeleo na Matumizi ya Kiswahili Bw. Kulwa Kindija kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa BAKITA. Bw. Kindija alieleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa sababu yanawajengea washiriki msingi mzuri katika kuzalisha machapisho bora na yenye tija kwa jamii.

Mafunzo hayo yaliwezeshwa na walimu watatu: Mhadhiri kutoka Taasisi ya Taaluma za Kiswahili - Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dkt. Leonard Bakize; Mchunguzi Lugha  Mkuu kutoka BAKITA, Dkt. Fatuma Mlaki; na Mchunguzi Lugha Mwandamizi kutoka BAKITA, Bw. Ambrose Mghanga.

Baadhi ya masuala yaliyofundishwa ni nafasi ya Kiswahili katika uandishi na uchapishaji bora wa vitabu, matumizi sahihi ya viakifishi (alama za uandishi), pamoja na ufasaha na usanifu wa lugha ya Kiswahili.

BAKITA linaendelea kutimiza dhamira yake ya kukuza, kuendeleza na kusimamia matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu ndani na nje ya nchi.