SALAMU ZA KATIBU MTENDAJI- BAKITA
Kwa niaba ya Menejimenti na Watumishi wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), ninayo furaha kuwakaribisha kwenye tovuti yetu mpya iliyoboreshwa ili muweze kupata taarifa za shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi yetu katika kukuza na kuendeleza Kiswahili kitaifa, kikanda na kimataifa.
Ninatumaini kuwa tovuti hii itakuwa ni njia sahihi itakayowezesha jamii kupata taarifa muhimu zinazohusu BAKITA na shughuli zake. Miongoni mwa shughuli hizo ni usanifishaji, Mafunzo ya Kiswahili kwa Wageni, Mafunzo ya Msasa ya Ukalimani kwa Vitendo, Uhariri wa Miswada mbalimbali, Ithibati ya Matini za Kitaaluma, Uandishi wa Vitabu mbalimbali na upatikanaji wake vikiwamo; Kamusi Kuu ya Kiswahili, Furahia Kiswahili, Mwongozo wa Ufundishaji Kiswahili kwa Wageni na vingine vingi. Aidha, Baraza linatoa huduma za Tafsiri, Ukalimani, Semina na Warsha kwa Waandishi wa Habari na Washereheshaji.
Vilevile, kupitia tovuti hii wadau, wapenzi na jamii kwa ujumla itapata elimu ya masuala mbalimbali yanayohusu matumizi fasaha na sanifu ya lugha ya Kiswahili, ambayo ni lugha yetu ya Taifa na moja ya lugha ya Afrika iliyopata mawanda mapana ya kutumika kimataifa. Nyota ya lugha hii imezidi kuangaza baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), kuitangaza lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za kimataifa kwa kuitengea siku maalumu ya kuadhimishwa duniani ambayo ni tarehe 7 Julai kila mwaka.
Ninatoa wito kwa wadau wote kuendelea kuitumia tovuti hii mara kwa mara na kuwasiliana nasi kwa maoni na ushauri kwa ajili ya kuboresha na kupata ufafanuzi zaidi kuhusu huduma zetu. “Hamadi ni iliyo kibindoni na Silaha ni iliyo mikononi” na kwetu ni Kswahili.
Tujivunie na Kukienzi Kiswahili, Moja ya Tunu za Taifa Letu.
Consolata P. Mushi
KATIBU MTENDAJI.