Tanzania emblem

Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania


Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)

Tanzania emblem

Kuhusu Sisi

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ni Shirika la Umma ambalo kwa kawaida huwa chini ya Wizara yenye dhamana ya Utamaduni. Baraza liliundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 27 ya mwaka 1967 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 1983 na 2016. Sheria hii inalipa Baraza mamlaka ya kusimamia na kuratibu shughuli za wadau wote wanaokuza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Baraza liliundwa kutokana na mapendekezo makuu ya Kamati iliyoundwa kwenye kikao cha wataalamu wa lugha kilichoitishwa na Waziri wa Elimu Disemba 1961. Lengo la kikao hicho lilikuwa ni kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuinua Kiswahili kama lugha ya Taifa. Baraza lilianza kazi na watumishi wanne katika ofisi za Wizara ya Elimu. Miongoni mwa kazi ya kwanza ya Baraza ilipendekezwa iwe kufasiri msamiati na misemo ya Sheria. Baadaye mwaka 1972, Baraza lilipata ofisi zake katika jengo la Shirika la Nyumba la Taifa, mtaa wa Samora na Azikiwe jijini Dar es Salaam, na mwaka 2012 Baraza lilihamia Kitalu Na.45 B, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

1.0  Dira

Kuwa taasisi yenye nguvu kisheria, kifedha na kutambulika kitaifa na kimataifa katika kuratibu na kusimamia maendeleo ya lugha ya Kiswahili.

2.0 Dhima

Kukuza, kuendeleza na kuhimiza matumizi fasaha na sanifu ya Kiswahili ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na wadau wengine.

Maadili ya Msingi

Ili BAKITA liweze kukaa katika mazingira wezeshi kwa ajili ya kufikia malengo yake ya kukuza na kusimamia maendeleo ya Kiswahili ndani na nje ya nchi, yafuatayo yatakuwa maadili yake ya msingi: -


  1. Kukuza ushiriki wa jamii: Kukuza ushiriki wa jamii kuhusu matumizi ya Kiswahili fasaha katika matumizi rasmi ya jamii
  2. Utendaji wa pamoja: Kufanya kazi kwa pamoja kama timu ili kufikia malengo ya Baraza na jamii kwa ujumla
  3. Kufanya kazi kwa bidii: Kuongeza juhudi katika kutoa huduma na kuzingatia ubora wa huduma zinazotolewa
  4. Uadilifu: Kuwa waadilifu na mfano wa kuigwa katika utendaji kazi
  5. Uwajibikaji: Kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa kuzingatia ukuzaji na uimarishaji wa lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi
  6. Matumizi mazuri ya rasilimali: Kutumia kwa uangalifu rasilimali za Baraza kwa manufaa na maendeleo ya lugha ya Kiswahili
  7. Uwazi: Kuzingatia uwazi wakati wa utekelezaji wa majukumu na kuwa tayari kupokea maoni ya jamii
  8. Kukubali mabadiliko: Kuwa tayari wakati wote ili kuendana na mabadiliko