Tanzania emblem

Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania


Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA)

Tanzania emblem

Nifanyeje?

Nifanyeje kupata Huduma zinazohusu Istilahi?

Mtu, shirika, taasisi au Kampuni ambayo inapata shida katika kupata istilahi za Kiswahili zinazoendana na shughuli zake iwasilishe istilahi hizo BAKITA kwa njia ya simu, barua pepe na kwa njia ya barua za kawaida. Aidha, mtu binafsi anaweza kuja BAKITA kupata ushauri wa chochote kinachohusiana na maneno mbalimbali ya Kiswahili.

Nifanyeje, kupata Huduma ya Tafsiri?

Kwa wale wanaotaka kutafsiriwa vyeti ni lazima watuletee nakala halisi na sio fotokopi. Kwa lugha ambazo Baraza lina wataalamu tunatafsiri kwa gharama ya Tsh 30,000 kwa cheti kimoja; Baraza linatumia wafasiri wa nje ambao wameidhinishwa kutafsiri lugha mbalimbali ambazo hatuna wataalamu wake ofisini. Mtaalamu wa nje anatafsiri kwa gharama atakazoelewana na mteja na kuandika jina na saini yake kwenye tafsiri na kisha mteja atatakiwa kuleta BAKITA kwa ajili ya kuthibitishiwa kwa kugongewa muhuri. Gharama za kugonga muhuri ni Tsh 10,000 kwa Mtanzania na Dola za Marekani 20 au Tsh 40,000 kwa mteja asiye Mtanzania. Kwa tafsiri ya miswada, vitabu n.k tunatoza Tsh 30,000 kwa ukurasa mmoja wenye maneno kuanzia 200 hadi 220. Mteja atatakiwa kuleta nakala mango (hard copy) na nakala tete (soft copy) kama anayo. Baraza litampatia Ankara Kifani (Proforma Invoice) ambapo atatakiwa kulipa asilimia 50 ya malipo yote kabla ya kazi kuanza, na kisha anapokuja kuchukua kazi atatakiwa kukamilisha asilimia 50 iliyobakia kabla ya kukabidhiwa kazi.

Nifanyeje ili niweze kupatiwa ithibati ya Kitabu?

Taratibu za kufuata wakati wa kumpatia mteja ithibati ya muswada au kitabu chake ni kama ifuatavyo:Fika ofisini na muswada wako ukiwa katika nakala mango.Muswada utakaguliwa idadi ya kurasa kwa ajili ya kulipia, ambapo gharama za malipo ni sh. 5000/= kwa kila ukurasa.Baada ya kulipia, muswada utasomwa na hatimaye mteja atarudishiwa kitabu chake na kwenda kuingiza marekebisho aliyoshauriwa.Ukisha kuingiza marekebisho hayo, atakirudisha tena kwa ajili ya kuhakikiwa kama umeingiza kwa usahihi marekebisho hayo, kadiri ya maelekezo uliyopewa.Ikiwa marekebisho hayo yatakuwa yameingizwa kama ilivyoshauriwa, kitabu au muswada utagongwa muhuri na hatimaye mteja atapatiwa cheti cha ithibati kwa ajili ya kitabu chake, kuwa kinafaa kutumika kwa wadau aliokusudia kwa kuwa sasa kina lugha iliyo fasaha na iliyothibitishwa.