Bonyeza Kuona Muundo wa Bakita!
Bofya uone kamati zilizopo za Baraza!


Siku ya Kiswahili

Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yalizinduliwa rasmi nchini Tanzania na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, Jumamosi ya tarehe 7 Januari mwaka 1995 katika Ukumbi wa IFM jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho haya yalikuwa ni utekelezaji wa wazo lililotolewa tarehe 31/7/1992 katika Kijiji cha Kwembe, Mkoa wa Dar es Salaam nyumbani kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Hayati Horace Kolimba. Siku hiyo ilifanyika hafla fupi ya kumpongeza Mzee Saadan Abdu Kandoro ambaye sasa ni marehemu kwa mchango wake alioutoa kwa kukikuza, kukiendeleza na kukitetea Kiswahili.

Kwenye hafla hiyo lilitolewa wazo kuwa kuwe na siku angalau moja kwa mwaka ya kuwakutanisha wapenzi mbalimbali wa Kiswahili, wafahamiane, wabadilishane mawazo kuhusu maendeleo ya Kiswahili na pia kuwatambua au kuwakumbuka watu mbalimbali waliochangia katika maendeleo ya Kiswahili. Watu hao hutunukiwa Nishani ya Shaaban Robert.


Madhumuni ya maadhimisho haya ni :

i. Kuirejesha hadhi ya Kiswahili kama Lugha ya Taifa ya Tanzania na kitambulisho cha Waafrika kwa ujumla;
ii. Kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala ya lugha na utamaduni ili washiriki kwa hali na mali katika ukuzaji na maendeleo ya Kiswahili;
iii. Kuzipa msukumo juhudi za kukuza Kiswahili na fasihi yake kwa kuwatambua na kuwaenzi wale wote waliochangia au wanaochangia sana katika juhudi hizo;
iv. Kuwakutanisha wakuzaji na wapenzi wa Kiswahili, wakiwemo watendaji wa asasi zinazokuza Kiswahili, walimu, waandishi wa vitabu, wafasiri na Wachapishaji, ili waweze kufahamiana na kubadilisha na mawazo na kupanga mikakati ya pamoja ya kuyatekeleza majukumu hayo;
v. Kuwakutanisha wakuzaji na wapenzi wa Kiswahili kutoka katika nchi zote zinazotumia Kiswahili;
vi. Kuikumbusha Serikali na Chama, kinachotawala kuhusu wajibu wao wa kuikuza, kuiendeleza na kuienzi Lugha ya Taifa;
vii. Kuimarisha ufundishaji na kujifunza Kiswahili kwa kuwatambua na kuwatunuku walimu na wanafunzi bora wa somo hilo.
viii. Kuanzisha mfuko wa kudumu wa kuendeleza Kiswahili na kukusanya fedha kwa ajili ya mfuko huo;


Asasi za Kiswahili zinazoandaa na kusimamia maadhimisho ni:

• Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) ambalo ndilo mratibu wakuu,
• Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
• Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni ya Zanzibar (TAKILUKI),
• Chama cha Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA),
• Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (UWAVITA),
• Taasisi ya Elimu Tanzania,
• Chuo Kikuu Huria,
• Ukurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni n.k.

Kila yanapofanyika maadhimisho haya nafasi ya Mwenyekiti huchukuliwa na asasi mojawapo inayokuza na kuendeleza Kiswahili. Katika Maadhimisho hayo siku moja hutengwa ili kufanya kongamano kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huo.

Kutokana na kukua na kuenea kwa Kiswahili ndani na nje ya Tanzania, maadhimisho haya huwashirikisha waalikwa wengine kutoka kwenye asasi za lugha za nchi mbalimbali duniani na kutoa mada.

Ilikubaliwa kwamba "Siku ya Kiswahili: itaadhimishwa Jumamosi ya Pili ya Januari kila mwaka. Siku hiyo imechaguliwa kwa kumbukumbu ya kumuenzi Marehemu Shaaban Robert. Yeye ni Mwandishi wa Vitabu maarufu aliyezaliwa tarehe Mosi Januari, 1909. Kwa kuwa tarehe Mosi Januari ni sikukuu ya Kimataifa haikuwa rahisi kufanya Maadhimisho hayo kwa tarehe hiyo na badala yake waandaaji hupanga tarehe nyingine mwafaka katika kipindi kisichozidi miezi miwili ili yasipoteze umuhimu wake.

• Maadhimisho ya kwanza yalifanyika mwaka 1995 mjini Dar es Salaam ambapo Profesa Euphrase Kezilahabi alitunukiwa Nishani ya Shaaban Robert.

• Maadhimisho ya pili yalifanyika mwaka 1997 huko Zanzibar. Haya yalikuwa ni ya kumuenzi Sitti Binti Saad.

• Maadhimisho ya tatu yalifanyika mwaka 1998 Dodoma, lengo lilikuwa ni kumuenzi Mathias Mnyampala.

• Maadhimisho ya nne yalifanyika mwaka 1999 jijini Dar es Salaam ambapo Profesa Penina Mhando Mlama alitunukiwa Nishani ya Shaaban Robert.

• Maadhimisho ya tano yalifanyika mwaka 2000 jijini Dar es Salaam ambapo Ndugu Omari Kiputiputi alitunukiwa nishani hiyo.

• Maadhimisho ya sita yalifanyika mwaka 2001 ambapo Nishani ya Shaaban Robert ilitolewa kwa Profesa Fikeni Senkoro.

• Maadhimisho ya saba yalifanyika mwaka 2003, jijini Dar es Salaam ambapo Tunzo ya Shaaban Robert ilitolewa kwa Profesa Mohamed Abdulla Mohamed.

• Maadhimisho ya nane yalifanyika mwaka 2005, Dar es Salaam na Tunzo ya Heshima ilitolewa kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati huo akiwa Waziri wa Mambo na Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kwa Wizara yake kwa kutetea kuingizwa kwa Kiswahili kuwa ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika.

• Maadhimisho ya tisa yalifanyika mwaka 2007, jijini Dar es Salaam na jopo la wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) walipewa tunzo kwa kuingiza matumizi ya Kiswahili kwenye Teknolojia ya Habari na Mawasiliano .

Lengo la siku hii ni kuwa siku ya Kitaifa ya Kiswahili, lakini mpaka sasa siku hii imekuwa ikiadhimishwa zaidi zaidi Dar es Salaam tu. Ingawa mwaka 1997/98 sherehe za siku hii zilifanyika Mjini Zanzibar/Dodoma.
Kutofanyika kwa siku hii katika sehemu mbalimbali za nchi, kunafanya siku hii kutofahamika vizuri kwa wananchi, hii imekuwa changamoto ambayo hatuna budi kuikabili na kuifanya siku hii iwe ya Kitaifa kwa kuwashirikisha wananchi na wadau wote wa Kiswahili


 
 
 

Content on this page requires a newer version of Adobe Flash Player.

Get Adobe Flash player