KAULIMBIU:  Kiswahili - Mhimili wa Umoja, Maendeleo ya Elimu na Uchumi.

Maswali Yanayoulizwa mara kwa mara


Baraza linatumia mbinu mbalimbali katika kuunda na kusanifisha maneno mapya ya Kiswahili, miongoni mwake ni kama vile: Utohozi m.f. kompyuta, Tafsiri m.f. free market- soko huria, Ufupishaji au akronimu m.f UKIMWI – Ukosefu wa Kinga Mwilini, Uhulutishaji; njia ambayo inahusiana sana na akronimu m.f. Chajio – Chakula cha jioni, Uambishaji m.f, a- na-som-a, som-w-a a-na-m-som-e-a, u-na-ye-m-som-e-a, Unyambulishaji m.f. som-a, som-e-a, som-w-a, som-ek-a, som-e-an-a. Uambatishaji m.f. mwanaanga, na Urudufishaji m.f. polepole. Aidha, katika uundaji wa maneno mapya mbinu nyingine inayotumika ni kurudi kwenye hazina ya Kiswahili chenyewe. Mbinu hii ni ile ya kuchota maneno kutoka kwenye lahaja za Kiswahili m.f. Kipemba, Kitumbatu, Kimrima, Kimvita n.k. Maneno pia hutafutwa katika lugha nyingine za kibantu, Kiafrika na ikitokea yamekosekana hutafutwa kwenye lugha nyingine za nje.

Istilahi zinazoundwa na Baraza husambazwa kwa watumiaji kwa njia zifuatazo: Vyombo vya habari: Baraza hutumia vyombo mbalimbali kama vile magazeti, redio na televisheni kusambaza maneno linayoyaunda. Kwa mfano Vipindi vya redio na Televisheni - Baraza huendesha vipindi mbalimbali vya Kiswahili katika televisheni na redio mbalimbali m.f. TBC Taifa, Redio One, Clouds, Redio Mlimani n.k. na televisheni kama vile TBC 1 ambapo hutumia fursa hiyo kunadi maneno mapya yaliyoundwa na pia kufuatilia matumizi yake. Baraza pia hutoa Makala mbalimbali katika gazeti la Habari leo, Makala hizo huelezea namna sahihi na miktadha ya utumiaji wa maneno mbalimbali ya Kiswahili. Mikusanyiko ya wadau mbalimbali wa Kiswahili: Baraza hutumia shughuli zinazowakutanisha wadau mbalimbali wa Kiswahili m.f. makongamano na warsha kunadi maneno mapya na pia kupata mwitiko wa matumizi ya maneno hayo kutoka kwa wadau hao. Vitabu: Baraza huandaa matoleo mbalimbali ya vitabu vyenye istilahi zake na hivyo wanajamii huweza kujifunza maneno hayo kupitia vitabu hivyo.

Baraza hufuatilia matumizi ya maneno linayoyaunda katika jamii kwa kusikiliza watumiaji lugha kwa ujumla pamoja na kusikiliza vyombo vya habari kuona iwapo maneno hayo yanatumika sawasawa.
Baraza huzuia upotoshaji wa lugha kwa kuelimisha jamii kuhusu utumiaji sahihi wa maneno. Hutoa elimu hiyo kupitia vyombo vya habari na wakati mwingine kuandikia barua taasisi, shirika au kampuni zinazoharibu lugha kwa kuonyesha maneno yanayobanangwa pamoja na masahihisho yake.

Baraza lina kamusi moja ya Kiswahili- Kiswahili ambayo ni Kamusi kuu ya Kiswahili, kamusi ya Istilahi za Kiswahili na kamusi nyingine ndogondogo za taaluma mbalimbali.

Baraza la Kiswahili la Taifa linafanya tafsiri ya lugha mbalimbali zinazozungumzwa duniani. Baadhi ya lugha hizo ni Kiswahili, Kiingereza, Kifanransa, Kijerumani, Kireno, Kiitaliano, Kiarabu, Kichina, Kijapani, Kirusi, Kihispaniola, Kituruki n.k

Hapana, BAKITA tunao wafasiri wa lugha za Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kireno na Kiarabu. Kwa lugha nyingine tunatumia wafasiri wa nje ambao sio waajiriwa wa Baraza. Wafasiri hao wameidhinishwa na wanafanya tafsiri kwa niaba ya Baraza.

Tunatoa huduma ya kutafsiri vyeti vya kuzaliwa, shule, ndoa, kifo n.k kwa lugha mbalimbali. Pia tunatoa huduma ya kutafsiri miswada mbalimbali, vitabu, mikataba n.k kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili na Kiswahili kwenda Kiingereza. Pia tunapitia na kuthibitisha tafsiri zilizofanywa na wafasiri wa nje.

Baraza pia linatoa huduma ya kupitia kazi ambazo zimeshatafsiriwa nje kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili kwa gharama ya Tsh 10,000 kwa ukurasa. Ili kupokea kazi hizo inabidi kwanza tuhakikishe aliyetafsiri ni mtaalamu na tunachofanya ni kurekebisha makosa madogo ya kisarufi na msamiati. Hatupokei kazi ambayo imetafsiriwa vibaya kiasi cha kutulazimu kuirudia upya.

Mteja haruhusiwi kutafsiri kazi yake yeye mwenyewe hata kama lugha anaifahamu, pia haruhusiwi kupeleka kwa mfasiri yeyote ambaye hajaidhinishwa na Baraza. Baraza linathibitisha na kugonga muhuri tafsiri ambazo zinatoka kwa wafasiri waliyoidhinishwa na Baraza tu.

Ndiyo, tunaratibu na kutoa huduma za Ukalimani na Tafsiri kwenye mikutano ya kitaifa na kimataifa na katika shughuli za makampuni, mashirika na watu binafsi. Mteja anapokuwa anahitaji wakalimani kwa ajili ya mkutano anawasiliana nasi na tunampa majina ya wakalimani ambao atawasiliana nao na watamueleza taratibu na gharama za kufanya ukalimani.

Tofauti iliyopo kati ya kuhariri na kutoa ithibati, ni kuwa kuhariri ni kungalia kama kanuni zote za uandishi zimezingatiwa kulingana na kazi ya uandishi iliyokusudiwa. Kama mwandishi alikusudia kuandika shairi, je amezingatia kanuni za uandishi wa shairi? Aidha kuhariri ni kuangalia pia matumizi sahihi ya alama mbalimbali za mandishi na maudhui na fani ya kazi yenyewe.

Kutoa ithibati ni kuangalia matumizi sahihi na fasaha ya lugha iliyotumika katika muswada husika kwa kuzingatia utamaduni, maadili na walengwa wa kazi hiyo. Ithibati haihusiki zaidi na maudhui na fani ya kazi inayohusika. Pamoja na hayo kazi hizi mbili haziachani sana kikanuni.

Kutokana na ufinyu wa bajeti, BAKITA halijaweza kuajiri wafanyakazi wengi zaidi ambao wangeweza kuwa na ofisi huko mikoani. Kwa maana hiyo basi, BAKITA halina ofisi mikoani. Baadhi ya majukumu ya BAKITA huko mikoani, hufanywa na maofisa utamaduni wa wilaya na mikoa.

Zote ni taasisi za Kiswahili, zinazoshughulika na maendeleo ya Kiswahili. Tofauti iliyopo ni kuwa BAKITA linaratibu shughuli zote zinazofanywa na taasisi nyingine zinazojishughulisha na maendeleo na ukuaji wa lugha ya kiswahili. TATAKI ni taasisi inayojishughulisha na kazi mbalimbali za ukuzaji wa Kiswahili kama ile kufanya utafiti, kusanifisha istilahi mbalimbali za Kiswahili kuandika kitabu kama ile kamusi na kuandaa walimu watakaofundisha Kiswahili katika ngazi mbalimbali za elimu kuanzia sekondari] hadi chuo kikuu.

BAKITA limekuwa likichukua hatua za dhati kabisa kukemea na kuelimisha wale wote wanaobananga Kiswahili kwa njia ya kuwafundisha ufasaha na matumizi sahihi ya Kiswahili kwa njia mbalimbali kama ile kipindi ya redio, televisheni, makongamano, warsha, semina na makala mbalimbali.

BAKITA limekuwa likifanya juhudi zifuatazo: kuishawishi serikali kuanzisha kituo kinachoshughulikia ufasaha wa lugha ya Kiswahili katika balozi zetu, kuishawishi serikali kutuma wataalamu wa kufundisha Kiswahili nje ya nchi, kufundisha Kiswahili kwa njia ya mitandao serikali, Kubadilishana wataalamu wa lugha na nchi nyingine ili tuweze kufundisha Kiswahili na sisi kujifunza lugha nyingine za kigeni.

Gharama za ithibati ni sh. 5,000/= kwa ukurasa, gharama hizi zinaweza kuongezeka kulingana na mabadiliko ya kiuchumi.

Kwa sasa BAKITA halihusiki kwa kiwango cha asilimia mia moja, bali mara tu kanuni zitakapopitishwa litawajibika mia kwa mia kushirikiana na wale wote wenye shughuli za kukuza Kiswahili.

Wasiliana na wanaidara wa idara husika, pia waweza kutumia simu ya BAKITA kuwasiliana na idara yoyote ili kupata maelekezo ya kina.

Ili kujifunza namna ya kuandika kazi mradi rejea viitabu mbalimbali ili ujifunze namna ya kuandika vizuri kazi mradi. Hata hiyo utaratibu wa kuandika kazi mradi hasa baada ya kukusanya taarifa unatakiwa kuandika.

  1. Jina la shule juu ya jalada
  2. Andika mada chini ya jina la shule
  3. Andika majina ya washiriki
  4. Kisha andika shukurani kuwashukuru wote waliofanikisha kazi hiyo
  5. Andika utangulizi ukielezea kuhusu kazi hiyo uliyoandika.
  6. Andika yaliyomo
  7. Anza kuandika mada zako
  8. Mwisho andika hitimisho, ukitoa mawazo yako kuhusu Kiswahili kwa ujumla au jambo linalohusu mada yako.

BAKITA lina mpango kabambe wa kufundisha Kiswahili kwa wageni. Hata hivyo hadi kufikia sasa Baraza limeshaandaa madarasa kwa ajili ya mradi huo. Pia tumeshaandaa muhtasari wa kufundishia. Tayari tumesharusha matangazo kwenye TV na Magazeti na tumeandaa vipeperushi na kuvisambaza kwenye balozi na hoteli mbalimbali jijini Dar es Salaam. Wengi wameonyesha nia ya kuanza kusoma Kiswahili. Tumeshaandika kitabu cha kufundishia Kiswahili kwa wageni. Tunawakaribisha wote wenye sifa ya kusoma Kiswahili kama kozi ya wageni waje wajiunge nasi.

Baraza hutumia vyombo vya habari pamoja na shughuli mbalimbali zinazohusisha wataalamu na wanajamii kwa ujumla kutangaza shughuli zake. Shughuli ambazo Baraza hutumia kutangaza kazi zake ni kama vile makongamano, warsha n.k. Baraza pia huandaa vipeperushi vinavyoeleza shughuli za Baraza na kuvisambaza kwa wanajamii.

BAKITA kirefu chake ni Baraza la Kiswahili la Taifa. Baraza liliundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 27 ya mwaka 1967 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1983.

Baraza hutoa huduma kwa watu walio mbali kwa njia ya simu, barua za kawaida na barua pepe.

Baraza huandaa semina maalumu kwa ajili ya waandishi wa habari na pia huandaa makongamano kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu utumiaji sahihi wa lugha. Aidha, Baraza limeandaa vitabu mbalimbali kikiwemo kitabu cha Mwongozo kwa Waandishi wa Kiswahili Sanifu ambacho maudhui yake yanalenga kuwasaidia waandishi kuandika kwa usahihi na kwa kuzingatia kanuni za uandishi.

Baraza limeandaa Kanuni za Sheria yake ambazo zitalipa mamlaka kisheria ya kuwatoza faini au kuwachukulia hatua zinazostahili wale wote wanaoharibu lugha. Hatua hizo zitachukuliwa baada ya Baraza kupitia hatua kadhaa za kuwaandikia au kuonana na wahusika ana kwa ana na kuwaeleza kuhusu jambo hilo. Ikiwa hilo litaendelea hata baada ya kupewa onyo mara tatu sheria itachukua mkondo wake.

Baraza limekusanya kanzi data ya wataalamu wa lugha ya Kiswahili katika uga wa ualimu, tafsiri na ukalimani. Pale kutakapokuwa na mahitaji, Baraza litatumia kanzi data hiyo kuwapata wahusika. Hata hivyo, Baraza linawahimiza Watanzania kuwa wepesi na wadadisi wa mambo ili kubaini haraka mahali panapohitajika wataalamu wa Kiswahili hususani kwa kutumia mitandao kutafuta nafasi hizo.

Baraza hutumia vyombo vya habari kuelimisha umma kuhusu usahihi wa lugha. Aidha, Baraza huandaa vitabu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kamusi, jarida la lugha yetu, Jifunze Kiswahili Uwafunze wengine ili kuwasaidia umma kutumia lugha kwa usahihi.

Baraza lina idara ya uchapishaji ambayo moja ya majukumu yake ni kuwasaidia waandishi chupukizi ili kuwajengea stadi nzuri za uandishi na kuwapa maelekezo ya namna ya kuandika kazi nzuri na zenye mvuto kwa jamii.

Mambo yanayoangaliwa ni:
i. Aina ya mswada.
ii. Muundo wa mswada.
iii. Maudhui ya mswada.
iv. Ufasaha wa lugha iliyotumika.
v. Usahihi wa alama za uandishi na matumizi ya herufi kubwa na ndogo.
vi. Wahusika waliotumika katika mswada.
vii. Walengwa wa mswada.
viii. Kufaa au kutofaa kwa mswada.

Mwandishi chipukizi apitie hatua zifuatazo:
i. Awe na uelewa wa kile anachotaka kukiandika (riwaya, tamthiliya, hadithi fupi, ushairi n.k.).
ii. Aandike rasimu ya kwanza.
iii. Awasiliane na BAKITA hii kwa ajili ya kuhaririwa na kupewa ushauri kuhusu kazi yake.
iv. Afanye marekebisho ya kazi yake kulingana na ushauri aliopewa na BAKITA.
v. Awasiliane na mchapishaji kwa ajili ya makubaliano ya kimkataba.
vi. Achapishe kazi yake.

Namba ya Kimataifa ya Kitabu (ISBN) hutolewa na Maktaba Kuu ya Taifa kwa kampuni/mashirika ya uchapishaji, mwandishi ataipata namba hiyo kwa mchapishaji atakayeingia naye mkataba wa kuchapisha kitabu chake.

Mchapishaji hushughulika na mchakato mzima wa kuandaa na kufuata taratibu za mswada kuwa kitabu pia kulinda haki za mwandishi. Mchapaji anapokea kazi iliyotayarishwa na mchapishaji na kuichapa kuwa kitabu.

BAKITA halichapishi vitabu vya waandishi mbalimbali badala yake huchapisha vitabu vyake lenyewe.

BAKITA linachapisha machapisho ya aina mbalimbali kama vile:
i. Kamusi za aina mbalimbali.
ii. Vitabu vya Sarufi, Fasihi na Historia ya Kiswahili.
iii. Vitabu vinavyohusiana na Matumizi ya kila siku ya lugha.
iv. Tafsiri Sanifu.
v. Vijitabu vya lugha tatu.
vi. Vitabu vya miongozo kwa waandishi.
vii. Vitabu vya Kiswahili kwa Wageni.

Machapisho ya BAKITA hupatikana katika sehemu zifuatazo:
i. Ofisi za BAKITA.
ii. Maonyesho, kama vile ya Sabasaba, Nanenane, Wiki ya Utumishi wa Umma n.k.
iii. Mikutano na Makongamano yanayohusu Lugha ya Kiswahili na Utamaduni wa Mtanzania.